Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) Tehran – Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Abbas Araqchi, katika mahojiano mapya na Shirika la Habari la IRNA amesisitiza kuwa, licha ya kuboreshwa kwa kiasi fulani hali ya usalama nchini Afghanistan, bado Taliban haijaheshimu haki za Waislamu wa Kishia, na haijajibu ipasavyo matarajio ya Iran katika masuala kadhaa muhimu kama vile haki ya maji, suala la wahamiaji na changamoto za kibenki.
Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la Kimataifa AhlulBayt (a.s) - ABNA: Araqchi alikosoa mwenendo wa Taliban katika kushughulikia masuala nyeti ya Afghanistan. Alisema kuwa Iran, licha ya kushirikiana kwa karibu na kundi hilo kwa ajili ya kulinda maslahi yake ya kitaifa, bado iko mbali na kulitambua rasmi serikali ya Taliban.
Akitaja changamoto kadhaa zinazohusiana na uhusiano wa Iran na Afghanistan - zikiwemo suala la wahamiaji, dawa za kulevya, ugaidi, usalama wa mipaka, biashara, tatizo la maji, lugha ya Kifarsi, na hasa usalama wa Waislamu wa Kishia - Araqchi alisema: “Hatuwezi kufumbia macho masuala haya.”
Waziri huyo wa mambo ya nje aliongeza kuwa, ingawa Taliban imechukua hatua fulani katika baadhi ya nyanja, bado imezembea pakubwa katika maeneo muhimu. Akibainisha zaidi alisema: “Kwa upande wa usalama, hali ya Waislamu wa Kishia imekuwa thabiti, lakini katika miaka michache iliyopita haki zao hazijaheshimiwa.”
Ikumbukwe kuwa, baada ya kurejea madarakani, Taliban ilifuta rasmi Sheria ya Hali ya Kiraia ya Waislamu wa Kishia, na kuondoa vitabu vyote vya Fiqh ya Ja’fari kutoka vyuo vikuu, shule na maktaba za serikali. Kundi hilo limekuwa likisisitiza kwamba sheria za Afghanistan lazima zitekelezwe kwa mujibu wa Fiqh ya Kihanifi pekee.
Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, Araqchi alizungumzia suala la haki ya maji ya Iran kutoka Mto Helmand, akisema kuwa hali imekuwa bora kidogo, lakini bado haijafikia kiwango kinachotarajiwa na Tehran. Pia aliongeza kuwa tatizo la huduma za kibenki kwa Wairani nchini Afghanistan bado halijapatiwa suluhisho.
Akigusia suala la wahamiaji, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alibainisha kwamba Iran na Taliban zimefikia makubaliano juu ya urejeo wa wahamiaji, ambapo takribani wahamiaji milioni moja wamerudishwa Afghanistan bila kuibua mgogoro katika uhusiano wa pande mbili.
Hata hivyo, alikumbusha kuwa hali ilikuwa ngumu na ya changamoto kubwa katika siku za mwanzo, kabla ya kushirikiana kwa karibu kati ya vikundi vya wananchi wa Afghanistan na Iran.
Your Comment